HUWEZI amini masikio yako pindi unapopata bahati ya kusimuliwa, kwani inavutia unapokuwa ukisimuliwa na yanavutia ukiyaona mwenyewe kwa macho yako maajabu ya Mwenyezi mungu yaliyosheheni ndani ya Kivutio cha Utalii cha Mapango ya Amboni.
Na pia ukipata bahati ya kusimuliwa na aliyetembelea mapango hayo na kujifunza kwa umakini, ama kwa hakika utatamani na utakupanda mzuka wa kufanya jitihada za hali na mali ili kufika na kujionea kwa macho, huku ukitamani kufahamu zaidi chanzo na Historia ya Makumbusho hayo ya Asili, yaliyo umbali wa Kilometa nane kutoka Tanga mjini.
Mapango haya ya Amboni yaliyopo Kata ya Kiomoi, Tarafa ya Chumbageni Wilaya na Mkoa wa Tanga kwakweli yanastahili kuwa moja ya vivutio vya utalii na muhimu kwa Taifa letu na hasa kutokana na vivutio vingi na historia ya mapango kuwa ni vya asili zaidi
vinavyomfanya mtu ashindwe kuamini yale anayoyaona na kusimuliwa mapangoni humo.
Mapango hayo yaliyotokana na mabadiliko ya nguvu za asili zilizobadilisha maumbile ya miamba ya Chokaa kipindi cha Jurasiki (JURASSIC PERIOD), miaka milioni 150, iliyopita kulingana na tafiti zilizokwishafanywa, eneo hilo la Mapango lilikuwa ni eneo la chini ya maji ya Bahari miaka milioni 20 iliyopita.
Inakadiliwa kuwa eneo hili lina ukubwa wa kilometa za mraba 234, lenye mazingira yam awe ya chokaa, pia ni eneo ambalo linapitiwa na mito na lenye uoto wa asili na mto ulio sifa kuu nne mojawapo ikiwa ni kutokauka maji kwa kipindi chote cha mwaka.
Katika mapango haya kuna namna ama njia mbalimbali zinazosemekana kusababisha mapango katika eneo hili, kutokana na utafiti uliofanywa na Mturi mwaka 1975, njia ya kwanza ni ile ya maji ya mvua yanayiochanganyika na hewa ya ‘Carbondioxide’ katika anga na kutengeneza tindikali (Carbonic Acid) yenye
uwezo wa kuyeyusha madini ya Calcium Carbonate, yanayounda sehemu kubwa ya miamba ya Chokaa.
Akielelezea maajabu haya kwa umakini mkubwa, Mwifadhi wa Mapango ya Amboni, Mwantum Hidary, mbele ya waandishi wa habari za michezo Taswa Fc, waliofika mapangoni hapo kujionea maajabu ya asili wakiwa katika ziara yao mkoa wa Tanga chini ya udhamini wa Kampuni ya simu za mkononi Vodacom, aliendelea kusema kuwa maji hayo yenye tindikali husababisha mabadiliko kidogo pindi yanapotelemka kuelekea ardhini.
Na Pindi yanapofika Meza ya maji (Water Table), yakiendelea kuongezeka huzidi kuchanganyika na ‘Carbondioxide’ iliyoko kwenye maji ya ardhini.
Kina cha maji kikiongezeka maji hayo yenye tindikali huwa na uwezo wa kuyeyusha maungio ya miamba katika sehemu laini zaidi za miamba na kusababisha nyufa ambazo huzidi kupanuliwa na maji yanayotembea na kuporomosha baadhi yam awe na kutengeneza mapango ama picha ya kitu ambavyo hadi leo
baadhi yake havijaweza kugunduliwa ni picha za vitu gani.
Njia nyingine ni kutokana na eneo hilo kusemekana lilikuwa chini ya usawa wa Bahari, yaani pembezoni mwa ufukwe, ambapo madimbwi ya bahari yalikuwa yakimomonyoa miamba ya chokaa na kusababisha Mapango na mara baada ya bahari kurudi nyuma kutokana na kupungua kwa kina cha maji katia eneo hili la mapango liliachwa likiwa kavu.
Msafara wa waandishi wa habari waliweza kuingia mapangoni humo ili kujionea wenywe baadhi ya maajabu ya asili yaliyokuwa yakisimuliwa na kukuta mambo yanayovutia zaidi ambayo kwakweli yanahitaji kusimamiwa na kutangazwa zaidi ili Serikali iweze kupatwa watalii wengi wa kigeni na kuiingizia kipato serikali.
Ama kwa hakika baadhi ya mambo ambayo huwezi kuamini unaposimuliwa na ukapatwa na mshangao pindi unapoyaona ni Ramani ya Afrika iliyojiunda kutokana na uwazi wa mapango na jiwe lililojichonga na kutengeneza picha ya kichwa cha Simba, ambavyo
vyote vipo kwenye mlango wa kuingilia mapangoni humo.
Na baadhi ya picha nyingine zilizojichora juu na pembeni mwa miamba kama Sanamu la Bikira Maria na Msikiti, ambavyo kila kimoja kimekaa upande wake na alama tosha za kuashiria kuwa ni picha uionayo mbele yako, huku msikiti ukiwa na badhi ya michoro inayoonekana kusomeka kama kitabu cha Quraan na kwa Bikira Maria kukiwa na alama ya kitabu kama bibria iliyofunuliwa.
Mengine ni pamoja na Bawa la ndege lililojichonga na kutengeneza picha halisi ya ndege ambayo unapoiona kabla
hujasimuliwa waweza kuhisi ni ndege aliyefia ama kunasa mahala hapo siku za nyuma.
Pamoja na hayo pia kuna picha ya Mamba, Unyayo wa Tembo, Mlima Kilimanjaro, Mlango wa Ndege ya abiria, Kochi lililojichonga mfano sofa, na kinachovutia zaidi ni picha ya Chui iliyojichora juu ya mwamba na unyayo wa kiatu ila mwisho wa yote ni Njia nyembamba.
Njia hii ilikuwa ni kivutio kwa kila mmoja wetu
aliyepia njia hiyo kwani ilituchukuwa kiasi cha dakika 20 kuwasubiri wenzetu ambao wamejaaliwa kuwa na miili mikubwa, waliolazimika kupita njia hiyo kwa staili ya kukaa na kusota kwa matako kutokana na wembamba wa njia hiyo ambapo baadhi yao walikuwa wakitoa hewa chafu kutokana na kujikunja ili kuweza kupita hapo.
Vilevile ndani ya Mapango haya kuna simulizi za Osale Otango, Samuel Otango na Paulo Hamis, ambao walikuwa wakitumia kituo namba tatu ndani ya mapango hayo kama sehemu ya kujificha kati ya mwaka 1952 na 56, wakati walipokuwa wakiendesha harakati za ukombozi wa watu weusi kutoka kwa walowezi na wakoloni wa kipindi hicho, na bila kusahau njia zilizomo mapangoni humo zinazoelekea Mombasa, Maweni na Mkoa wa Kilimanjaro.
Haya yote yametokana na njia mbalimbali zilizoelezewa kutokea kwa mapango haya, hata hivyo hadi hii leo haijulikania mapango haya yaligunduliwa lini, bali taarifa zilizopo zinaonyeshja kwamba watu wa makabila
yaliyoishi jirani na eneoa hilo, Wabondei, Wasambaa, Wadigo na Wasegeju wamekuwa wakiyatumia kwa ajili ya matambiko ya mizimu tangu karne ya 16.
Eneo hili la mapango kwa wakati huo likijulikana kama eneo la Mzimu wa Mabavu, kwa hivi sasa hutumika na baadhi ya watu wanaoamini nguvu za mizimu kutoka sehemu mbalimbali za Afrika Mashariki ambao huja kuomba na kutambika katika vijipango mbalimbali mapangoni humo.
Serikali iliyachukua mapango hayo kutoka kwa iliyokuwa Kampuni ya Kigeni ya Amboni Limited, mwaka 1922 iliyokuwa ikimiliki mashamba ya mkonge katika maeneo ya Tanga, ambayo likuwa ikiyatumia mapango hayo kama sehemu ya kupumzikia.
Baadhi ya vivutio vingine ni maeneo yaliyotengwa maalum kwa ajili ya kuomba au kutambikia mizimu, ambapo ukifika maeneo hayo utaona vitu vingi vinavyohusiana na imani za kijadi.
Pia kuna miamba mingo yenye maumbo ya kuvutia kama, Meli, Mamba, na mchoro wa Chui uliotokana na uchafu wa
vumbi na udongo ambao umenywea pamoja na maji ya mvua na hatimaye kuganda katika paa la pango.
Kuna miamba inayokua au kuongezeka kutokana na mabadiliko kikemikali katika miamba ya chokaa, ambapo mabadiliko haya hutokana na maji yenye tindikali kuyeyusha madini ya ‘Calcium Carbonate’, na kuyahamisha na kuyarundika katika katika (Stalactive) inayoelekea (Stalagmite).
Kulingana utafiti ulioishafanywa, umeonyesha kuwa miamba ya aina hii huongezeka kukua kwa kasi zaidi kipindi cha mvua kuliko kipindi cha kiangazi, na katika kipindi cha miaka kumi iliyopita, ukuaji wake umekuwa milimeta 0.5 na kila baada ya miaka 100. na kuwa iliwahi kuongezeka kwa kasi ya milimeta 7 katika kila miaka 100 kipindi cha kati ya miaka 38000 na 34000 (38 & 34Ka).
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni