MUZIKI WA MALIMBA

MUZIKI WETU

HABARI? MPENZI MSOMAJI KARIBU KATIKA KURASA HII MAALUM KWA AJIRI YA HABARI ZIHUSUZO UTALII NA UTAMADUNI KUTOKA KATIKA VISIWA VYA MARASHI YA KARAFU ZANZIBAR ,NA MAENEO JIRANI YANAYOFANANA TABIA NA VISIWA HIVI +255 713 15 33 48

Jumatano, 1 Juni 2022

TAARIFA KWA UMMA WATALII WALIOINGIA NCHINI, KIPINDI CHA JANUARI - APRILI, 2022

 

Taarifa ya mwenendo wa watalii waliongia nchini ni miongoni mwa taarifa za muda
mfupi (high-frequency data) zinazotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu kwa mujibu
wa Sheria ya Takwimu SURA 351.
Idadi ya Watalii Walioingia Nchini Januari - April 2022
Katika kipindi cha kuanzia mwezi Januari hadi Aprili 2022, idadi ya watalii 367,632
kutoka nje ya nchi walitembelea vivutio mbalimbali vya utalii ikilinganishwa na
watalii 275,097 walioingia nchini kipindi kama hicho mwaka 2021. Hili ni ongezeko la
watalii 92,535 sawa na asilimia 33.6 (Jedwali Na. 1). Kati ya watalii 367,632 walioingia
nchini, watalii 124,212 waliingia nchini kupitia Zanzibar ambao ni sawa na asilimia
33.8 ya watalii wote.

 
Watalii walioingia nchini mwezi Aprili 2022, waliongezeka hadi 78,784 kutoka watalii
43,966 walioingia nchini mwezi Aprili 2021. Idadi ya watalii walioongezeka walikuwa
34,818 sawa na asilimia 79.2. Ongezeko hilo limetokana na nchi nyingi duniani
kuondoa zuio la kusafiri kufuatia kupungua kwa hali ya maambukizi ya UVIKO-19
na juhudi za Serikali kuendelea kutangaza vivutio vya utalii nchini.
Jedwali Na. 1: Idadi ya Watalii Walioingia Nchini Kuanzia Januari Hadi Aprili 2022
2021 2022 Ongezeko Badiliko (%)
Januari 79,116 94,128 15,012 19.0
Februari 79,730 100,936 21,206 26.6
Machi 72,285 93,784 21,499 29.7
Aprili 43,966 78,784 34,818 79.2
Jumla 275,097 367,632 92,535 33.6
Chanzo: Idara ya Uhamiaji, 2022
Idadi ya Watalii Walioingia Nchini Kabla na Baada ya UVIKO-19
Idadi ya watalii walioingia nchini mwaka 2019 walikuwa 1,510,151 ambapo idadi
kubwa zaidi ya watalii 160,296 waliingia nchini mwezi Desemba 2019. Baada ya dunia
kukumbwa na UVIKO-19, nchi nyingi ziliweka vikwazo vya kusafiri vilivyosababisha
idadi ya watalii walioingia nchini kupungua hadi 620,867 mwaka 2020 ambapo idadi
ndogo zaidi ya watalii 7,105 waliiingia nchini mwezi Aprili 2020. Mwaka 2021, idadi
ya watalii walioingia nchini iliongezeka hadi 922,692, sawa na asilimia 48.6.

Kumb. Na. BA.275/376/01/20 Tarehe: 18 Mei, 2022
Mawasiliano yote yafanyike kupitia kwa Mtakwimu Mkuu wa Serikali
Matarajio ya Idadi ya Watalii Wanaoingia Nchini
Idadi ya watalii wanaotarajiwa kuingia nchini itaongezeka zaidi ya idadi iliyokuwepo
kabla ya UVIKO-19 kutokana na juhudi mbalimbali za Serikali za kutangaza vivutio
vya utalii ambavyo ni pamoja na mbuga za wanyama, fukwe za bahari, Mlima
Kilimanjaro, uwindaji na utalii wa kitamaduni. Aidha, kukamilika na kuanza
kurushwa kwa filamu ya Tanzania, the Royal Tour iliyozinduliwa na Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan imeiwezesha
Dunia kuitambua Tanzania. Kuongezeka kwa viwango vya ukuaji wa shughuli za
uchumi zinazohusiana na sekta ya utalii zinazojumuisha Sanaa na Burudani (asilimia
11.7) na Malazi na Huduma za Chakula (asilimia 11.3) ni miongoni mwa viashiria
vinavyoonesha kuendelea kuimarika kwa sekta ya utalii nchini.

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni